UNHCR imesema kwamba imepokea ripoti za mamia ya wakimbizi kurudishwa Myanmar katika muda wa miezi miwili iliyopita.
Shirika hilo limesema kwamba mpango huo unakiuka sheria ya kimataifa na kuwaweka wakimbizi katika hatari kubwa.
Msemaji wa UNHCR Shabia Mantoo amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba watu hawawezi kuendelea kurudishwa sehemu wasiyoitaka, ambapo maisha yao yapo hatarini.
“UNHCR inaendelea kuitaka serikali ya Malaysia kuacha kuwarudisha kwa lazima wakimbizi nchini Myanmar ambao wameikimbia nchi hiyo kwa sababu ya usalama wao. Hatua ya kuwarudisha huko inawaweka katika hatari kubwa. Watu wanaokimbia Myanmar wanastahili kupewa hifadhi na kulindwa dhidi ya udhalilishaji. Raia wa Myanmar wanaoishi nje ya nchi yao hawastahili kulazimishwa kurudi nchini mwao wakati wanatafuta ulinzi wa kimataifa."
Tukio la hivi karibuni ni la mhamiaji ambaye alirudishwa Myanmar, Oktoba 21, licha ya shirika la UNHCR kuingilia kati na kutaka hatua hiyo kutochukuliwa.
Myanmar inakabiliwa na migogoro ya vita.
Msemaji wa serikali ya kijeshi ya Myanmar, wizara ya mambo ya ndani na wizara ya mambo ya nje hawajasema lolote kuhusiana na madai hayo licha ya ombi la waandishi wa habari.
Ubalozi wa Myanmar nchini Malaysia umeandika ujumbe wa Facebook kwamba wahamiaji 150, raia wa Myanmar, wamerejeshwa nyumbani Oktoba 6, kwa kutumia usafiri wa ndege kwa ushirikiano na maafisa wa uhamiaji wa Malaysia.