Wakimbizi wakimbilia Sudan, mapigano yaongezeka Ethiopia

PM ABiy AHmed Interview

Mapigano makali yanaendelea Tigray, Ethiopia, wakimbizi wakikimbilia Sudan huku Umoja wa Afrika ukiendelea kutoa wito wa kusitishwa mapigano hayo.

Jeshi la Ethiopia linaendelea kushambulia makundi ya wapiganaji katika eneo hilo, baada ya viongozi wa Tigray kukaidi mamlaka ya waziri mkuu Abiy Ahmed.

Karibu watu 2,500 wamekimbilia Sudan kutoka Ethiopia kufuatia mapigano hayo katika eneo la Tigray huku maafisa wakielezea wasiwasi wao kwamba huenda idadi ya watu wanaokimbia mapigano hayo ikaongezeka kwa kasi.

Mamia ya watu wamekufa kutokana na mashambulizi ya angani huku hali ya wasiwasi ikiongezeka kwamba huenda Ethiopia ikarudi tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokana na uhasama mkubwa uliopo kwa sasa kati ya jamii ya Tigray na Oromo.

Maawsiliano yamekatwa katika eneo la Tigray.

Shirika la habari la serikali limeripoti kwamba wanajeshi wa serikali wamedhibithi uwanja wa ndege wa Humera, karibu na mpaka na Sudan na Eritrea.

Shirika la habari la FANA, linaloshirikiana na serikali, limeripoti kwamba wanajeshi 17 wamekamatwa kwa kutatiza mfumo wa mawasiliano unaotumika na wanajeshi wa serikali ya jimbo la Tigray na kuhatarisha usalama wa jeshi la jimbo hilo TPLF.

Abiy, ambaye alishinda tuzo la amani la Nobel mwaka 2019, aliamurisha mashambulizi ya angani na kutuma wanajeshi Tigray wiki iliyopita, akishutumu jeshi la TPLF kwa kushambulia kambi ya jeshi.

Utawala wa Tigray unadaia kwamba serikali ya Abiy inawakandamiza na ilichukua hatua za kidikteta kuahirisha uchaguzi mkuu.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC