Tangu serikali ya Sudan Kusini kuikamata kambi ya waasi Kusini Magharibi mwa nchi wiki iliyopita, mamia ya wakimbizi wameendelea kumiminika kwenye nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Miongoni mwao huenda wamo waasi, na jeshi la Kongo ambalo linahofia kuenea kwa vita na kuingia nchini mwao, linakamata watu wote wanaoshukiwa kuwa wapiganaji.
Wakimbizi hata hivyo wanasema kuwa vijana wasiokuwa na hatia pia wamekamatwa wakati wa msako huo.
Ni vigumu kujua ni washukiwa wangapi waliokamatwa kufikia sasa.
Afisa mmoja wa serikali ya Kongo aliyezungumza kwa misingi ya kutotajwa jina kwa sababu haruhusiwi kuongea na wanahabari, alisema washukiwa tisa wako rumande ya kijeshi.
Viongozi kwenye kambi moja ya wakimbizi wamesema waasi 17 ndio waliokamatwa kufikia sasa.