Migogoro ya kikabila pamoja na mapigano kati ya majeshi ya usalama na makundi yenye silaha katika baadhi ya maeneo ya kusini mashariki mwa Congo, ilipelekea wimbi kubwa la wahamiaji kwelekea Zambia mwaka 2017.
Sasa hivi hali kwenye jimbo la Haut Katanga ambako ghasia hizo zilishuhudiwa inasemekana kuwa tulivu na hivyo kuruhusu kurejea kwa salama kwa wakazi waliokimbia makwao.
Inasemekana kwamba karibu wakimbizi 5,000 wa DRC wamefanya uamuzi wa kurejea makwao kwa msaada wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR pamoja na serikali ya Zambia.
Kundi la kwanza la watu 100 limeondoka Jumanne kwenye eneo la Mantapala kwenye jimbo la Laupala nchini Zambia likielekea kwenye kijiji cha Pweto kilichoko kwenye jimbo la Haut Katanga DRC.
Msemaji wa UNHCR Babar Baloch amesema kwamba hali ya usalama kwenye eneo hilo imeimarika kiasi cha kuruhusu wakimbizi kurejea kwao kwa njia salama na yenye heshima.
UNHCR imesema kwamba zoezi hilo litaendelea hadi mwaka ujao mpaka pale wote wanaotaka kurejea makwao watakapo pata nafasi ya kufanya hivyo.