Matukio ya mwisho ya kesi ya uhalifu wa fedha ya Donald Trump mjini New York nchini Marekani yalijitokeza Jumanne huku wakili wa utetezi wa Trump na mwendesha mashtaka wakijibizana vikali iwapo rais huyo wa zamani wa Marekani alifanya kinyume cha sheria kushawishi matokeo ya uchaguzi ya mwaka 2016 uliompeleka White House.
“Rais Trump hana hatia”, Todd Blanche alisema katika hoja yake iliyochukua saa tatu ya kufunga mjadala. “Hakufanya uhalifu wowote, na mwanasheria wa wilaya hajatimiza wajibu wake wa ushahidi”. Blanche alitoa wito kwa jopo la baraza la mahakama lenye watu 12 wanaosikiliza kesi hiyo ili kutoa “uamuzi wa haraka na rahisi usio na hatia”.
Lakini mwendesha mashtaka Joshua Steinglass aliliambia baraza la mahakama lenye wanaume saba na wanawake watano, kwamba Trump, ambaye ni rais wa kwanza kuwahi kushtakiwa kwa makosa ya jinai, alijihusisha na njama ya “kupotosha uchaguzi wa mwaka 2016”.