Kwa mujibu wa wakili wake, Cliff Ombeta, Miguna, ambaye amezuiliwa kwenye uwanja huo tangu alipowasili nchini hapo jana, alipelekewa fomu hizo na maafisa wa idara ya uhamiaji, baada ya kukataa kuwasilisha cheti chake cha kusafiria.
Gazeti la Daily Nation limeripoti kwamba kufikia alasiri ya leo saa za Kenya, hatima ya Miguna bado haikuwa ikijulikana na kwamba bado yuko kwenye uwanja wa ndege.
Idara ya uhamiaji ya Kenya inasisitiza kwamba Miguna alipoteza uraia wake mwaka wa 1988 alipochukua uraia wa Canada kwa sababu wakati huo, katiba ya Kenya haikuruhusu uraia pacha.
Jumanne, idara hiyo ilitoa taarifa iliyosema kuwa kwamba ni sharti aombe upya uraia huo kwa mujibu wa sheria. Afisa mwandamizi wa idara hiyo, Joseph Munywoki, alithibitisha kwamba maafisa wake walikuwa wamempelekea Miguna fomu za kuomba uraia.
Vurugu zilizuka Jumatatu usiku pale maafisa wa usalama walipompomlazimisha wakili huyo kuabiri ndege ya shirika la ndege la Emirates, lakini akakataa kusafiri na kusema kuwa hawezi kulazimishwa kufanya hivyo.
Miguna, ambaye amejitangaza kuwa kiongozi wa vuguvugu la National Resistance Movement (NRM- Kenya), amekuwa akiishi uhamishoni tangu maafisa wa polisi walipomlazimisha kuabiri ndege katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi mapema mwezi Februari, kwa madai kwamba yeye si raia wa Kenya.
Mapema mwezi Februari, serikali ya Kenya iliwasilisha hoja mahakamani na kudai kuwa Miguna aliukana rasmi uraia wake na kwa hivyo hastaili kudai kuwa Mkenya.
Lakini mwanasiasa huyo mwenye utata ameshikilia kwamba katiba ya Kenya inaeleza bayana kuwa mtu aliyezaliwa katika nchi hiyo hawezi kupoteza uraia wake.
Sakata hiyo inajiri chini ya wiki tatu baada ya rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta Kukutana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga na kukubaliana kushirikiana pamoja kutafuta uwianio wa kitaifa.
Kabla ya kulazimishwa kwenda uhamishoni, Miguna alikuwa amekamatwa na kuzuiliwa na polisi kwa takriban siku tano kwa tuhuma kwamba alitoa kiapo - kinyume na sheria - kwa kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, mbali na kuwa mwanachama wa vuguvugu la NRM lililopigwa marufuku.
Lakini licha ya mahakama moja mjini Nairobi kumtaka afikishwe mbele ya jaji, polisi walimuwasilisha mbele ya hakimu katika mji ulio mbali na mji mkuu wa Kenya, na baadaye wakampeleka moja kwa moja hadi kwenye uwanja wa ndege, na kuwondosha nchini.
Tangu wakati huo, Miguna amekuwa akishiriki mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari na kufanya mikutano na Wakenya wanaoishi nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kutembelea miji kadhaa ya Canada, Marekani na Uingereza.