Wananchi wa Kenya wamepiga kura leo kuamua endapo watakubali katiba mpya iliyopendekezwa nchini humo.
Wananchi wa Kenya wamepiga kura ya maoni kuamua endapo watakubali katiba mpya iliyopendekezwa ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza mivutano ya kisiasa na kikabila nchini humo.
Makisio ya awali yanaonyesha kuwa huenda asilimia 60 ya wapiga kura walijitokeza kushiriki katika upigaji kura ambao kwa jumla ulifanyika kwa amani. Hadi majira ya jioni hakukuwa na ripoti za vurugu zozote kubwa nchini.
Maafisa wanasema kazi ya kuhesabu kura itaanza usiku wa manane Jumatano, saa chache baada ya upigaji kura kufungwa.
Utafiti wa maoni ya watu awali ulionyesha kuwa sehemu kubwa ya wananchi wanaelekea kuunga mkono mapendekezo hayo ya katiba ambayo pia yanaungwa mkono na Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga.