Hii ni kufuatia uchaguzi uliofanyika Jumanne wiki hii katika taifa hilo la Afrika Mashariki.
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amekiri kwamba zoezi la kuhakiki kura za urais, linaloendelea katika ukumbi wa Bomas of Kenya, linajikokota na akatangaza kanuni mbadala za kwendelea na zoezi hilo katika juhudi za kuharakisha mchakato huo.
Tayari matokeo ya wawakilishi mbalimbali kote nchini yametangazwa, huku magavana sita kati ya 47 waliotangazwa washindi wakiwa ni wanawake, ikilinganishwa na watatu pekee katika serikali iliyopita.
“Baadhi ya maafisa waliosimamia uchaguzi katika viwango vya maeneo bunge wamekuwa katika ukumbi huu kwa siku tatu wakisubiri kuwasilisha nyaraka zao za Fomu 34B.
Hilo halikubaliki,” alisema Chebukati alipowahutubia waliokuwepo ukumbini Jumamosi alasiri, na kuagiza kwamba idadi ya madawati yanayotumika kudhibitisha matokeo hayo yaongezwe na mawakala wampelekee nyaraka zao moja kwa moja.
Mwanasiasa mkongwe Raila Odinga na Naibu wa Rais William Ruto ndio waliokuwa wakiongoza katika kura za awali zilizotangazwa na tume hiyo.
Wagombea wengine walikuwa ni George Wajackoyah na David Mwaure Waihiga.
Tume hiyo inaruhusiwa hadi siku saba kutangaza matokeo baada ya uchaguzi kufanyika.
Baadhi ya viongozi wa kisiasa waliendelea kuwarai wafuasi wao na Wakenya kwa jumla kuwa na subra. Kwa mujibu wa katiba ya Kenya, ni mwanyekiti wa IEBC pekee ambaye ametwikwa jukumu la kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa rais.