100 wakamatwa kwa kutoa heshima kwa kifo cha kiongozi wa upinzani Russia, Navalny

Zaidi ya watu 100 wanashikiliwa nchini Russia, kwa kuweka mashada ya maua wakati wa kutoa heshima zao kwa kiongozi wa upinzani Alexey Navalny, kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la Associated Press (AP), ya Jumamosi.

Mashada ya maua yaliondolewa baadaye na wafanyakazi waliosimamiwa na polisi AP imesema.

Shirika la utetezi wa haki za binadamu la Russia, OVD-Info, limesema lilisema katika taarifa yake kwamba Navalny, alihamishwa kwenye mojawapo ya magereza yenye ukatili mkubwa zaidi nchini Russia, ambalo lipo ng’ambo ya ukanda wa mzunguko wa Arctic.

“Wakati wa miezi 37 akiwa kizuizini, Navalny, alitumia siku 296 katika chumba cha adhabu cha gereza chenye ukatili,” taarifa hiyo ilisema.

Rais wa Marekani, Joe Biden, Ijumaa aliongelea kifo cha Navalny, kwa kumlaumu moja kwa moja rais wa Russia, Vladimir Putin, na kutumia kifo hicho kulikemea baraza la wawakilishi la Marekani kwa kushikilia ufadhili kwa Ukraine.