Watoa huduma ya mtandao nchini Myanmar ikiwemo kampuni ya mawasiliano ya MPT inayomilikiwa na serikali wamezuiwa fursa ya huduma zinazomilikiwa na kampuni ya Facebook nchini humo siku ya Alhamis kwa saa za huko, siku kadhaa baada ya viongozi wa jeshi kuchukua madaraka katika njia ya mapinduzi.
Barua iliyochapishwa mtandaoni na wizara ya mawasiliano na habari nchini humo imesema Facebook itazuiwa huduma zake hadi Februari 7 kwa ajili ya kuweka hali ya utulivu nchini humo. Baadhi ya watumiaji wa huduma za mtandao huko Myanmar wanaripoti hawakuweza kupata fursa kadhaa za huduma zinazotolewa na Facebook.
Kundi linalofuatilia masuala ya mtandao la NetBlocks, linathibitisha kampuni ya mawasiliano ya MPT inayomilikiwa na serikali ambayo inasema ina watumiaji milioni 23, ilizuia mawasiliano ya Facebook pamoja na huduma nyingine kama vile Messenger, Instagram na WhatsApp.
Kampuni ya Telenor Asa ya Norway ilisema iliizuia Facebook tu kufuatia agizo hilo. Msemaji wa Facebook, Andy Stone anakiri kuwepo hitilafu hizo.