Sherehe za Arbaini ni kuadhimisha mwisho wa siku 40 ya kuomboleza mauaji ya Imam Hussein, mjukuu wa Mtume Mohamed SAW, katika karne ya saba, aliyeuliwa na wapiganaji wa Khalifa Yazid. Hilo ndilo tukio muhimu linalosemekana lilianzisha madhahemu ya kishia katika uislamu.
Mkusanyiko huo ambao ni moja wapo ya mikusanyiko mikubwa ya kidini duniani hufanyika kila mwaka, ambapo waumini wanaume kwa wanawake kutoka pembe mbali mabli za dunia hukusanyika Karbala ambako Imam Hussein na kaka yake Abbas walizikwa.
Wasimamizi wa sherehe hiyo wanasema baada ya miaka miwili ya shughuli zote kusitishwa kwa sababu ya janga la COVID, wameshuhudia watu milioni 21.2 waliowasili wiki hii katika mji huo ulioko kati kati ya Iraq kuhudhuria sherehe hizo.
Miongoni mwa waumini hao milioni 5 wametokea nchi za nje na milioni 3 kutoka nchi jirani ya Iran, ikiwa ni idadi kubwa kabisa ya mahujaji kuwahi kushuhudiwa kutoka nchi hiyo, kulingana na maafisa wa nchi hizo mbili.
Katika sherehe hizo wanaume hujipiga kifuwani kwa minyororo wakiandamana hadi makaburi mawili ya maimamu hao, huku wakiimba kaswida za kidini. Ina aminika kitendo hicho ni hatua ya kujiadhibu kutokana na mauaji ya wajukuu hao wawili wa Mtume Mohamed.
Waumini wengine wanabeba bendera nyeusi na mabango yenye picha ya Imam Hussein.