Mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa na kimataifa yapo katika harakati za kutoa misaada ya kuokoa maisha kwa walio nusurika na kimbunga Mocha, katika nchi za Bangladesh na Myanmar.
Wanaotoa misaada ya kibinadamu wanaonyesha kuchoshwa na vikwazo vya ukiritimba na kisiasa vilivyowekwa na watawala wa kijeshi wa Myanmar.
Kimbunga Mocha ni chenye nguvu zaidi kuwahi kukumba Ghuba ya Bengal katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, kilisababisha maporomoko matatu ya ardhi Jumapili, kung'oa miti na paa pamoja na kukata nyaya za umeme huku upepo wa kilomita 250 kwa saa ukivuma katika eneo hilo.
Eneo la kwanza kushambuliwa na kimbunga ni Jimbo la Rakhine, ambako Waislamu wa Rohingya 600,000 wanaishi, huku 150,000 kati yao wakiwa katika makambi ya wakimbizi wa ndani. Maporomoko ya ardhi yalifuatiwa katika Jimbo la Chin na eneo la Kaskazini la Sagaing.