Wahandishi wa Nigeria wamesema jengo la ghorofa 21 lililoporomoka mjini Lagos mapema mwezi huu awali lilipangwa kuwa na ghorofa sita pekee, kabla ya ghorofa nyingine kuongezwa kwenye jengo hilo.
Jengo hilo refu lilikuwa bado linaendelea kujengwa katika wilaya ya Ikoyi wakati lilipomomoka hapo Novemba mosi na kusababisha darzeni moja ya wafanyakazi kwenye eneo hilo kukwama na wengine wakiwa ndani. Takribani watu 45 akiwemo mmiliki wa jengo hilo walifariki, huku wengine 15 wakitolewa wakiwa hai kutoka kwenye vifusi kulingana na idadi ya hivi karibuni iliyotolewa na serikali ya jimbo.
Mashirika ya dharura awali yalikuwa yameweka idadi ya watu waliofariki kuwa 42 lakini mamlaka za serikali zilisema wiki iliyopita kwamba maiti tatu zaidi zilipatikana chini ya vifusi.
Ingawa serikali imeunda jopo la kubaini chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo ndani ya mwezi mmoja, taasisi ya wahandisi wa majengo nchini Nigeria ilisema kuwa tofauti katika muundo wa awali ndio wa kulaumiwa. Rais wa taasisi hiyo Kehinde Osifala alisema katika taarifa yake ya Jumanne.