Katika ripoti iliyoandikwa na UNHCR na baraza la wakimbizi la Udachi, maelfu ya wakimbizi na wahamiaji hutaabika sana mikononi mwa maafisa wa usalama, ikiwemo kupigwa na kunyanyaswa kingono na hata kuuawa.
Waandishi wa ripoti hiyo waliwahoji wakimbizi na wahamiaji 16,000.
Katika kikao na waandishi wa Hhbari mjini Geneva, mjumbe maalum wa UNHCR Vincent Cochetel, amesema kwamba “katika visa 47, waathiriwa waliripoti kwamba maafisa wa usalama ndio wanaoongoza katika manyanayso dhidi ya wakimbizi na wahamiaji, japo tulikuwa tunadhania kwamba wahusika wakuu walikuwa ni wafanyabiashara ya magendo na walanguzi wa biandamu”.
Ripoti hiyo inataka mataifa kuwajibika katika kukabiliana na manyanyaso dhidi ya wahamiaji na wakimbizi.
UNHCR imeripoti kwamba watu 1,750 walikufa kati ya mwaka 2018 na 2019 wakijaribu kufika ulaya kupitia bahari ya mediterania, na kwamba huenda idadi hiyo ikawa kubwa kuliko ya inavyodhaniwa.
“Kuna familia zinatafuta watu wao kwenye pwani hiyo na hakuna majibu ya kuwapa,” imesema ripoti hiyo.
Katika miezi ya hivi karibuni, mamia ya wahamiaji wamekamatwa baharini na kurejeshwa Libya licha ya vita vinavyoendelea nchini humo.
Jumatatu wiki hii, maafisa wa Libya waliwapiga risasi na kuua wahamiaji watatu kutoka Sudan waliokuwa wanajaribu kuhepa kuwekwa katika kizuizi maalum, baada ya kukakamatwa katika bahari ya Mediterania wakijaribu kuelekea Ulaya.
Libya, ambayo inakabiliwa na vita vikali, ni njia muhimu sana kwa wahamiaji kutoka nchi kadhaa za Afrika wanaojaribu kufika Ulaya.
Karibu wahamiaji 654 wanazuiliwa nchini Libya baada ya kukamatwa baharini. Wengi wao hawapati huduma za afya na wanaishi katika hali mbaya.
-Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC