Wahadhiri Kenya wafikia makubaliano na serikali

Chuo Kikuu cha Nairobi

Baada ya vuta nikuvute kati ya serikali ya Kenya na Wahadhiri wa vyuo vikuu nchini, hatimaye muafaka umepatikana baada ya wahadhiri kupewa nyongeza ya asilimia 17.5.

Nyongeza hiyo ya mishahara yao inakwenda sambamba na muafaka kufikiwa kati ya pande hizo mbili kuwa mkataba wa makubaliano wa 2013-17 uanze kutekelezwa.

Wahadhiri wa vyuo vikuu walikuwa kwenye mgomo wa siku hamsini na nne wakishinikiza serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kuwapa nyongeza ya mshahara pamoja na kuisawazisha.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili ameripoti kuwa hatimaye "moshi mweupe" umefuka katika mazungumzo kati ya Serikali na Muungano wa Wahadhiri wa Vyuo Vikuu nchini UASU.

Amesema kuwa katika siku hamsini na nne kulikuwa na hali tata katika vyuo vikuu nchini, huku wahadhiri kutoka vyuo vikuu vya umma kote nchini wakiwa katika mgomo.

Mwandishi wetu anatujuza ya kuwa katika makubaliano ambayo yameweza kufikiwa Jumatatu na ambayo yatatambulishwa rasmi kisheria kesho mahakamani, wahadhiri wamepewa nyongeza ya mishahara yenye asilimia 17.5 pamoja na nyongeza ya marupurupu yenye asilimia 3.9 ambayo ni shilingi bilioni sita.

Aidha, mkataba wa makubaliano uliofikiwa Julai mosi mwaka 2013 utaanza kutekelezwa. Hii inaamanisha kuwa wahadhiri wataanza kulipwa nyongeza hii kuanzia kipindi ambacho mkataba huu ulitiwa sahihi mwaka 2013.

Mohamed Mwachiti, mojawapo wa viongozi wakuu katika muungano wa UASU walioshiriki mazungumzo haya na serikali, anaieleza idhaa ya sauti ya Amerika kuwa wahadhiri katika viwango mbalimbali watapata nyongeza hii.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya