Wafungwa zaidi ya 900 watoroka jela Congo.

Wafungwa zaidi ya 900 watoroka jela Congo.

Watu wawili wauwawa katika shmbulizi la kumtorosha jela kiongozi muasi pamoja na wafungwa zaidi ya 900.

Afisa mmoja katika jamhuri ya kidemokrasia ya Congo anasema watu wenye silaha wameshambulia jela moja katika eneo la kusini mashariki la Katanga na kuuwa watu wawili na kuruhusu karibu wafungwa 1000 kutoroka.

Waziri wa mambo ya ndani wa Katanga Dikanga Kazadi amesema washambuliaji 8 waliwashambulia walinzi katika jela kwenye mji wa Lubumbashi Jumatano katika mpango wa kumtoa kifungoni kiongozi wa waasi. Maafisa wanasema mmoja kati ya watu wawili waliouwawa alikuwa mlinzi, wakati mwingine alikuwa mgeni kwenye jela hiyo.

Kazadi amesema wafungwa 967 wametoroka ikiwa ni pamoja na kiongozi muasi Gedeon Mutanga aliyeshitakiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na mahakama moja ya kijeshi ya Congo 2009.

Amesema Polisi baadaye walikamata tena wafungwa kiasi cha 150.

Mutanga ni kiongozi wa zamani wa wanamgambo wa Mai Mai huko Katanga , kituo kikuu cha uchimbaji madini huko Congo.