Kuvuja kwa kemikali mapema Alhamisi, kwenye kitengo cha uhandisi cha uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kuala Lumpur, Malaysia, kumesababisha takriban watu 20 kuumwa, afisa wa huduma ya dharura amesema.
Jumla ya watu 6 wamepatiwa matibabu kwenye kliniki ya uwanja huo, huku wengine 13 wakipelekwa kwenye kituo cha afya na mmoja kwenye hospitali ya umma, afisa wa dharura wa eneo hilo Muhammad Nur Khairi Samsumin amesema katika taarifa.
Waathirika wote 20 walikuwa ni wafanyakazi kwenye makampuni matatu yaliyopo kwenye uwanja huo, wengi wao wakidai kuhisi kizunguzungu baada ya kupumua kemikali hiyo.
Hata hivyo tukio hilo halikuathiri safari za ndege kwenye uwanja huo mkubwa zaidi nchini Malaysia. Maafisa wa dharura wametumwa kwenye uwanja huo, ingawa sababu za kuvuja kwa kemikali hiyo hazijatolewa.