Wafanyakazi wa afya wasitisha mgomo kwa muda, Zimbabwe

Wafanyakazu wa afya wa Zimbabwe wakiwa kwenye mgomo uliositishwa kwa muda Jumamosi.

Wafanyakazi wa afya wa Zimbabwe wamesitisha mgomo wa siku tano wa kudai malipo na kuanza kurudi kazini Jumamosi.

Hata hivyo viongozi wa vyama vya wafanyakazi wameonya kuwa wataanza tena mgomo huo ikiwa serikali itashindwa kutoa mapendekezo ya kuongeza mishahara ndani ya wiki mbili.

Maelfu ya madaktari na wauguzi katika hospitali za serikali kwenye taifa hilo la kusini mwa Afrika wanadai nyongeza ya mishahara na mafao mengine yalipwe kwa kutumia dola ya Marekani kutokana na kushuka kwa thamani ya sarafu ya Zimbabwe .

Wafanyakazi hao walianza mgomo Jumatatu baada ya kukataa mapendekezo ya Serikali ya kuongeza mishahara yao mara mbili zaidi, wakisema ongezeko la asilimia 100 haliwezi hata kufidia mfumuko wa bei wa kila mwaka ambao ulipanda hadi asilimia 131.7 mwezi Mei.

Chini ya sheria ya Zimbabwe wafanyakazi kwenye sekta muhimu ni lazima wapate kibali cha kufanya mgomo lakini viongozi wa jumuiya wamesema hawahitaji kufanya hivyo kama wataamua kuanza tena mgomo wiki ijayo.

Jumuiya ya wauguzi wa Zimbabwe wamesema wafanyakazi wengi wa afya wa Zimbabwe wanalipwa elfu 20 fedha ya Zimbabwe ambayo ni sawa na dola 53 ya Marekani kwa mwezi.