Maelfu ya waandamanaji waliingia mitaani kote nchini Ufaransa siku ya Alhamis kwa siku moja ya mgomo wa nchi nzima wakipinga pendekezo la serikali la mageuzi ya ajira ambapo itafanya iwe rahisi kwa waajiri, kuajiri na kuwafukuza wafanyakazi na kudhoofisha nguvu za umoja wa wafanyakazi.
Waandamanaji mjini Paris walipambana na polisi huku maelfu kadhaa walioandamana wakipiga kelele kwa maneno ya kupinga serikali kote mjini Paris wakidai kwamba serikali imebadilisha mwelekeo wa muswada wa ajira. Waandamanaji walikutana na gesi ya kutoa machozi wakati polisi walipopambana na kundi la waandamanaji waliojifunika uso.
Polisi waliwakamata watu 77 wakati maelfu walipoandamana kutoka eneo la Bastille kuelekea mashariki mwa Paris. Hali imekuwa ya mvutano katika mji wa bandari wa Le Havre nchini Ufaransa mahala ambako wafanyakazi wanazuia moja ya maeneo makuu ya mafuta nchini humo.
Maelfu ya makuli waliingia katika eneo mbele ya halmashauri ya mji hapo Alhamis na kuwasha mabomu ya moshi kwenye eneo zima. Wakati huo huo viwanda vya nyuklia 11 kati ya 58 huko Ufaransa vilikumbwa na ukosefu wa umeme usiotarajiwa wakati wafanyakazi walipojiunga kwenye maandamano.