Wafanyabiashara na raia wa Gabon waliokwama Cameroon waridhishwa na utawala wa kijeshi kufungua mipaka

Msemaji wa Kamati ya Mpito na Urejeshaji wa Taasisi (CTRI), Kanali Ulrich Manfoumbi Manfoumbi (kati) akisoma taarifa kwenye televisheni. AFPTV

Wafanyabiashara wa Afrika ya kati katika eneo maarufu huko Kye-Ossi, kwenye mpaka wa kusini wa Cameroon na Gabon na Equatorial Guinea, wanasema wanafuraha kuwa uongozi mpya wa Gabon umeamuru kufunguliwa tena kwa mipaka yake.

Wafanyabiashara wa Afrika ya Kati na raia wa Gabon ambao walikwama huko Kye-Ossi, mji wa kusini mwa Cameroon, wameridhishwa na utawala wa kijeshi kufungua tena mipaka ambayo ilifungwa baada ya mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Rais Omar Ali Bongo Ondimba hivi karibuni.

Wafanyabiashara wengi katika eneo maarufu huko Kye-Ossi, kwenye mpaka wa kusini mwa Cameroon na Gabon na Equatorial Guinea, wanasema wanafuraha kuwa uongozi mpya wa Gabon umeamuru kufunguliwa tena kwa mipaka yake.

Jumamosi, utawala wa kijeshi wa Gabon ulisema unafungua tena mipaka, siku tatu baada ya kuifunga wakati wa mapinduzi ya kijeshi ambapo Rais Ali Bongo Ondimba aliondolewa mamlakani.

Dereva wa gari kubwa raia wa Gabon, Nguea Rene mwenye umri wa miaka 26, ambaye alikuwa amekwama nchini Cameroon, anasema anasubiri wanajeshi wa mpakani kuheshimu maelekezo ya utawala wa kijeshi na kufungua tena mpaka ili aweze kuwa na familia yake katika mji mkuu wa Gabon, Libreville .

Nguea anasema alikwenda Cameroon kununua vipuri vya magari lakini hakuweza kurejea nyumbani kwasababu mpaka ulikuwa umefungwa. Nguea anasema ombi lake kwa uongozi mpya nchini Gabon ni kufungua nafasi za ajira kwa raia, hasa vijana wadogo, ambao wanaishi maisha ya taabu.

Wanajeshi kadhaa wa serikali ya Gabon bado wako upande wa mpaka wa Gabon. Mamia ya magari magodo na makubwa yamekwama pande zote mbili za mpaka.

Viongozi wa Gabon walisema kwenye televisheni ya taifa kwamba mipaka ya ardhini, bahari na anga ilikuwa imefunguliwa kwasababu utawala unataka kuimarisha utawala wa sheria na kuendeleza uhusiano mzuri na majirani zao na nchi zote duniani.

Kossock Pierre ni mhadhiri katika chuo kikuu cha Omar Bongo mjini Libreville. Anasema kufungwa kwa mpaka na amri ya kutotoka nje nchini Gabon ilikuwa sehemu ya hatua za usalama zilizochukuliwa kuilinda nchi kutokana na hali yoyote ambayo haikutarajiwa baada ya Ali Bongo kuondolewa madarakani. Anasema serikali ya Gabon ni vyema iwe na uangalifu mkubwa kwa mipaka yake kwa kuwaruhusu wanajeshi waangalie nani anaingia na nani anatoka.

Kossoch anasema itakuwa ni makosa kudhani kwamba Ali Bongo na baba yake, Omer Bongo, ambao walitawala Gabon kwa zaidi ya miaka 56 kuwa hawana marafiki ambao walinufaika kutokana uzalishaji mafuta wa taifa hilo na wanataka himaya ya Bongo kushikilia madaraka. Kossock anasema raia na jeshi kwa kiasi kikubwa wanaunga mkono mabadiliko katika uongozi wa Gabon na taifa hilo la Afrika ya Kati litachukua tahadhari kwa jaribio lolote ambalo litaandaliwa na taifa jirani ili kumrejesha Bongo katika mamlaka.

Mwaka 2019, Gabon ilifunga kivuko vya mpakani na nchi jirani ya Cameroon baada ya wanajeshi waasi kuonekana kwenye televisheni ya taifa wakitangaza kuwa wamefanya mapinduzi dhidi ya Rais Ali Bongo kurejesha demokrasia. Serikali ya Gabon baadaye ilisema kuwa imepata udhibiti wa nchi na kuwakamata wanajeshi waasi saba.

Uchaguzi wa Gabon ulifanyika Agosti 26, Ali Bongo aliwania kuchaguliwa tena. Matokeo ya uchaguzi yaliashiria Albert Ondo Ossa mwenye umri wa miaka 69, waziri wa zamani na profesa wa chuo kikuu, alishinda kura.

Lakini Kituo cha Uchaguzi cha Gabon kilitangaza Ali Bongo mshindi kwa asilimia 64 ya kura. Huku kukiwa na mkanganyiko, jeshi la Gabon lilitangaza limekamata madaraka na kumuweka Ali Bongo kwenye kizuizi cha nyumbani.

Haijulikani itachukua muda gani kuondoa msongamano wa magari kwenye mipaka mara kila kitu kitapokuwa kinafanya kazi tena na magari kuanza kutembea.