Marekani: Wademokrat wataka "ukiukaji wa haki za waandamanaji" Oregon ufanyiwe uchunguzi

Makabiliano kati ya waandamanaji na maafisa wa serikali kuu ya Marekani wa kulinda usalama. Julai 17, 2020.

Wajumbe watatu wa cheo cha juu ndani ya chama cha Democratic nchini Marekani na ambao pia ni wabunge walisema Jumapili kwamba wanataka uchunguzi ufanyike kuhusu iwapo maafisa wa idara moja ya serikali kuu walitumia vibaya mamlaka ya dharura wakati walipowasaka na kuwakamata waandamanaji waliokuwa watulivu wakipinga serikali wiki iliyopita katika mji wa Portland, jimbo la Oregon.

Wawakilishi Jerold Nadler wa New York, Carolyn Maloney wa New York na Bennie Thompson wa Mississippi walituma barua Jumapili kwenda kwa mkaguzi mkuu wa wizara ya sheria na usalama wa ndani, wakisema wanaelezea wasiwasi wao kwa utawala wa Trump kutumia maafisa wa idara ya serikali kuu kulinda usalama kukiuka haki za raia na katiba ya nchi.

Kulingana na barua hiyo, maafisa wa serikali kuu wakiwa kwenye gari lisilo namba wakiwakamata waandamanaji kwenye mitaa ya Portland.

Waandamanaji mjini Bend, Oregon wakipinga kile wanachokiita "unyamavu wa Wazungu"

“Maafisa wengine wamewakamata, kuwachunguza na kuwaweka kizuizini washukiwa usiku wa manane kabla ya kuwasomea haki zao. Ni ukiukaji wa katiba,” ilieleza barua hiyo.

-Imetayarishwa na Mkamiti Kibayasi, VOA, Washington DC