Wabunge hao hali kadhalika wanamtaka Waziri wa elimu, Fred Matiang’i, kujiuzulu katika kipindi cha wiki moja, la sivyo watachukua hatua ya kuwasilisha mswada bungeni wa kumuondoa madarakani wakati bunge litakapoanza shughuli zake.
Watunga sheria Mark Nyamita (Uriri), Caleb Amisi (Saboti) na Walter Owino (Awendo) pia wanataka Bunge likutane ili kujadili matokeo hayo ya mitihani.
Wabunge hao wanasema kuwa wamemwandikia Spika wa Bunge la Taifa Justin Muturi wakimtaka awaite kwa dharura ili waweze kujadili ukweli juu ya mtihani huo.
Wanamtuhumu Matiang’i kwa "kutoa matokeo ambayo hayajafanyiwa marekebisho yoyote, jambo lililopelekea wanafunzi wengi kufeli."
Zaidi ya asilimia 80 ya wanafunzi hawakuweza kufikia alama ya C+ na juu ya hapo katika mtihani wa kidato cha nne 2017. Alama ya C+ ndiyo kiwango cha chini kabisa kumruhusu mwanafunzi kujiunga na chuo kikuu.
“Hatuwezi kuwalaumu wanafunzi kwa kukabiliwa na mustakabali mbaya kwa kuwa Matiang’i amekuwa na haraka ya kutoa matokeo,” Nyamita alisema katika mkutano wake na waandishi wa habari Nairobi.
Hata hivyo, waziri Matiang'i amesisitiza kuwa ameridhishwa na matokeo hayo.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha Citizen mjini Nairobi hivi karibuni, Matiang'i alisema Wakenya wamekuwa wakiishi maisha ya uongo kuhusiana na suala la mitihani na ni wakati muafaka wa kusema ukweli.
"Wakati umefika hivi sasa kwetu sisi kuelezana na kukabiliana na ukweli," alisema.
Your browser doesn’t support HTML5