Bunge jipya Tanzania halitakuwa na sauti ya upinzani

Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Hai na kiongozi wa upinzani bungeni Freeman Mbowe.

Watanzania wamekwenda kwenye sanduku la kura Oktoba 28, 2020 na kuchagua viongozi wao, rais Jamhuri ya Muungano, wabunge pamoja na madiwani watakaowaongoza kwa miaka mitano ijayo.

Uchaguzi huo umeshuhudia chama tawala cha CCM kikijizolea viti vingi vya bunge na udiwani na kumpa tena rais John Magufuli muhula wa pili kwa asilimai 84.

Huku wabunge wengi maarufu wa upinzani waliokuwa wameonyesha ushindani mkubwa dhidi ya chama tawala kwenye uchaguzi katika miaka ya nyuma wakiangushwa kwa kishindo kikubwa.

Wabunge hao machachari ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhoji utendaji wa serikali ndani ya bunge la jamhuri ni pamoja aliyekuwa kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni Freeman Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti wa CHADEMA, kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe na aliyekuwa mbunge wa Kigoma mjini na Mchungaji Peter Msigwa aliyekuwa mbunge wa Iringa Mjini.

Aliyekuwa mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi au Sugu, aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kawe Halima Mdee na aliyekuwa mbunge wa Tarime John Heche miongoni mwa wengine.

Sura ya bunge lijalo la Tanzania litakuwa kwa kiasi kikubwa la chama kimoja kwani mpaka sasa ni wabunge wawili tu ndiyo waliofanikiwa kupenya na kuingia katika bunge hili.

Wabunge hawa watakumbukwa kwa michango yao na mijadala mikali katika bunge la jamhuri ya muungano wakifichua ufisadi na pia kuibana serikali katika masuala mbali mbali.

Msigwa alisikika mwaka 2017 akisema “huu ni wakati wa kuibana serikali na kuonyesha utofauti wa mihimili akieleza kuwa wabunge wenzake wanadhani serikali ina nguvu kuliko wao, wakati ni kinyume chake ilihitajika bunge liiwajibishe serikali kwa matumizi ya fedha ambayo wabunge hawakuidhinisha aliongeza.

John Heche alikuwa kinara wa kutetea wafanyakazi wa uchimbaji migodi mkoani Mara akitetea haki zao na kutaka mauaji yakomeshwe katika maeneo hayo.Akitaka serikali itenge maeneo kwa wananchi.

Naye aliyekuwa Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi au Sugu alikuwa maarufu kama mtetezi wa wamachinga katika jiji la Mbeya na atakumbukwa kwa juhudi zake za kuwatetea wakulima wa Mbeya na sakata la vitambulisho akisema wasilazimishwe kununua vitambulisho hivyo kwani wakulima hao sio wamachinga. Alidai kuwa vitambulisho hivyo vilivyotolewa na rais Magufuli vinawaumiza watu wake.

Wabunge hawa wa upinzani pia watakumbukwa kwa visa mbali mbali bungeni kimojawapo mwaka 2017 kiliwahusisha Esta Bulaya na Halima Mdee walipewa adhabu kwa kudharau mamlaka ya spika na kufungiwa baada ya kuingilia kati hatua ya kutolewa nje mbunge wa upinzani John Mnyika kutokana na utovu wa nidhamu huku Esta Bulaya akiwahamasisha wabunge wa kambi ya upinzani watoke nje ambao walifuata matakwa yake.

Naye kiongozi wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe Dk Benson Bagonza anasema ushindi huo wa CCM safari hii unawashangaza walioshinda na walioshindwa ikiwa ni pamoja na wapiga kura akimnukuu baba wa taifa hilo la Tanzania marehem Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema “tumetoka mfumo wa chama kimoja kwenda vyama vingi na tukishindwa vingi, hatuwezi tena kurudi chama kimoja bali tutaelekea mfumo mwingine labda udikteta na kwa uchaguzi huu anasema tunarudi katika mfumo wa chama kimoja.