Wabunge wa Somalia waliendelwa na zowezi la kumchagua rais mpya Jumapili, licha ya kusikika milipuko karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mogadishu, uliyo chini ya ulinzi mkali.
Kati ya wagombea 39 walowasilisha majina yao, wabunge wamefanikiwa kupunguza idadi hiyo na kuwachagua wakongwe wanne wa kisiasa, wakati wa duru ya kwanza ya uchaguzi.
Kiongozi mpya anatazamiwa kutangazwa Jumapili usiku.
Wagombea wane walobaki ni Rais wa jimbo la Puntland Said Abdulahi Deni, Rais Mohamed Abdullahi Mohamed anaegombania kiti chake, rais wa zamani Hassan Sheikh Mohamed na waziri mkuu wa zamani Hassan Ali Khaire.
Nusu dazeni ya wakazi na mwandishi wa habari wa Reuters walisikia milio iliyokuwa kama ya mizinga. Wasomali wamezoea mara kwa mara kuona mashambulizi kwenye majengo ya seikali na maeneo mingine ambayo yanafanywa na waasi wa kiislamu.
"Nilihesabu milio mitatu mikubwa ya makombora ikitua katika mwelekeo wa uwanja wa ndege. Tulishtushwa sana kusikia milio ya makombora wakati Mogadishu iko katika amri ya kutotoka nje. Nani alikuwa akiyafyatua?” alisema Halima Ibrahim, mmoja wa wakazi,.
Hakuna ripoti zozote kuhusu uharibifu wowote au vifo.
Uchaguzi huo unachukuliwa ni muhimu sana kuweza kuhakikisha mzozo wa kisiasa unamalizika na kuruhusu msaada wa kigeni kuendelea kupelekwa katika nchi hiyo inayokumbwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa karibu miongo mitatu sasa.
Wabunge wanapiga kura ndani ya hema kubwa chini ya ulinzi mkali kwenye uwanja wa ndege na hadi hivi sasa hakuna taarifa juu ya matokeo ya uchaguzi huo. Amri ya kutotoka nje imetangazwa katika mji mkuu huo hadi jumatatu asubuhi.