Wabunge wa baraza la wawakilishi la Marekani, Jumanne walianza kutafakari muswada wa kuongeza ukomo wa deni la serekali la dola trilioni 31.4 mpaka mapema 2025 kuwezesha ukopaji zaidi na kufanikisha kulipwa kwa madeni.
Hayo yanafanyika wakati maafisa wa White House wanakaribisha makubaliano yaliyofikiwa kupitia mfululizo wa majadiliano na kuiondoa Marekani kwenye uwezekano wa kushindwa kulipa madeni kabla ya muda uliobashiriwa wa kutokuwa na fedha siku kadhaa zijazo.
Mkurugenzi wa ofisi ya utawala na bajeti, Shalanda Young, amesema kwamba jambo hilo halikuwa rahisi, na kwamba wanatoa mwito kwa pande zote mbili kupitisha muswada na kuupeleka mezani kwa rais.
Rais wa Marekani, ambaye ni Mdemokrat, na spika wa baraza la wawakilishi kutoka chama cha Republikan ambao walikubaliana mpango wa kuongeza ukomo wa deni wanaamini wana kura zakutosha za kuupitisha.