Wabunge wa Marekani huenda wakafanya kazi mpaka sikukuu ya Krismasi wiki ijayo wakijaribu kushauriana juu ya makubaliano kuhusu usalama wa mpaka ili kupata kura za Warepublikan kwa ajili ya kupitisha msaada zaidi kwa Ukraine.
Kiongozi wa walio wengi katika baraza la Seneti, Chuck Schumer, aliwaambia wanahabari Jumanne kwamba ingawa ana matumaini kuhusu maendeleo ya mashauriano, wabunge wanahitaji muda zaidi.
“Masuala katika jambo hili ni mengi kwa sababu hili sio jambo ambalo bunge imelishughulikia katika kipindi kirefu na tunajua kuwa hii haitakuwa rahisi kufanya,” alisema Mdemokrat katika Seneti.
Kiongozi wa walio Wachache katika Seneti, Mitch McConnell, pia alikubali uwepo wa ugumu huo, na kusema mara ya mwisho mswaada wa uhamiaji na usalama wa mpaka kuwa sheria ilikuwa mwishoni mwa miaka ya 1980.