Waasi wazingira mji mkuu wa Bangui Jamhuri ya Afrika ya kati. Mapigano yaongezeka

Jamhuri ya Afrika ya kati imetangaza hali ya dharura, wakati wanajeshi wa serikali na umoja wa mataifa wakipigana kujaribu kuwafukuza waasi wanaotaka kuipindua serikali.

Waasi wanadhibithi theluthi tatu ya Jamhuri ya Afrika ya kati, na wamezingira mji mkuu wa Bangui.

Ujumbe wa umoja wa mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya kati umesema kwamba nchi hiyo iko katika hatari kubwa sana.

Makundi ya waasi yameukataa ushindi wa rais Faustin Archange Touadera katika uchaguzi mkuu wa mwezi Desemba.

Maafisa serikalini wanamshutumu aliyekuwa rais Francois Bozize, aliyezuiwa kushiriki katika uchaguzi wa Desemba 27, kuwaunga mkono waasi hao.

Bozize, ambaye aliingia madarakani mwaka 2003 kabla ya kupinduliwa mwaka 2013, amekana madai hayo.

Zaidi ya watu 60,000 wamekimbilia nchi jirani kutokana na mapigano yanayoendelea.