Maafisa wa kundi hilo la waasi wamesema mabaki ya kombora hilo la Jeshi la Ukraine aina ya Tochka ambalo lilirushwa na kuanguka katikati ya mji wa Donesk, limesababisha vifo vya Zaidi ya darzeni ya watu na kujeruhi wengine wengi.
Wizara ya afya ya jimbo hilo lililojitenga na Ukraine imesema katika taarifa “ Vifo 16 vimerekodiwa na kuongeza kuwa watu wengine 23 walijeruhiwa”.
Vituo vya matangazo vya eneo hilo lililojitenga vimesambaza picha na video baada ya shambulio hilo, zikionyesha magari yaliyoungua, miili iliyojaa barabarani, na uharibifu wa nje ya maduka.
Shirika la habari la AFP limesema haliwezi kuthibitisha idadi ya vifo iliyotangazwa na maafisa wa eneo hilo lililojitenga, ambalo linadhibitiwa na waasi wanaoungwa mkono na Moscow tangu mwaka wa 2014.