Waasi wachukua mji muhimu Mali.

Waunga mkono wa waasi wa kijeshi wakishiriki katika maandamano dhidi ya jumuiya ya uchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bamako.

Baada ya waasi kuteka mji mwingine viongozi wa mapinduzi wanakumbana na shinikizo kali la kimataifa kuachia madaraka

Waasi wameingia katika mji wa Kidal leo siku moja baada ya kufanya shambulizi katika mji huo wa ndani , makao makuu ya mkoa wa Kidal kaskazini mwa Mali.

Ripoti kutoka eneo hilo zinasema waasi wa MNLA walisaidiwa na kundi moja la kiislam lijulikanalo kama Ansar Edine.

Katika mji mkuu Bamako kiongozi wa mapinduzi ya wiki iliyopita amesema nchi yake inahitaji msaada wa nje ili kuwazuia waasi na kulinda heshima ya mipaka ya Mali. Kapteni Amadou Sanogo aliwaambia waandishi wa habari Ijumaa kwamba hali ni mbaya.

Viongozi wa mapinduzi wanakumbana na shinikizo kali la kimataifa kuachia madaraka. Alhamisi jumuiya ya uchumi ya mataifa ya Afrika magharibi ililipa kundi hilo la kijeshi siku tatu kurudisha utawala wa kikatiba .

Hata hivyo Rami Ajebewa afisa wa juu wa ECOWAS aliiambia VOA kwamba jumuiya hiyo ya kikanda itakubali suluhisho ambalo halimrudishi rais Amadou Toumani Toure madarakani.