Vikosi vinavyotaka kujitenga vya Tuareg, vimepinga mpango wa mazungumzo ya wote ya Mali kwa ajili ya amani na maafikiano uliowekwa na utawala wa kijeshi baada ya miezi kadhaa ya ghasia baina ya waasi na jeshi.
Mapigano baina ya wanamgambo wanaotaka kujitenga, na vikosi vya serekali ya Mali yalianza tena mwezi Agosti, baada ya miaka minane ya utulivu wakati pande hizo mbili ziliposhindwa kushughulikia upungufu uliotokana na kujiondoa kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa.
Katika hotuba ya mwaka mpya Jumapili, mtawala wa kijeshi kanali Assimi Goita, ametangaza kuanzishwa mazungumzo ya moja kwa moja ya kuleta amani, na muafaka ili kuondoa mzozo wa kijamii na migogoro ya jamii na jamii.
Amesema mazungumzo yatajikita kuhusu utawala wa kitaifa wa mchakato wa amani.