Hapa katika chumba cha habari cha Evidencias, mjini Maputo, Msumbiji, Reginaldo Tchambule na timu yake wanafanya kazi ya kuweka rekodi sawa katika jitihada za kupambana na upotoshaji na taarifa za uongo.
Ushirikiano Katika Kupambana na Upotoshaji
Yeye na mwenzake Nelson Mucandze, wanasema walianzisha pamoja gazeti na lile la mtandaoni miaka minne iliyopita kwa sababu mashirika mengine mengi hayakuwa yakikagua ukweli au kutumia taarifa na uchambuzi katika kuripoti kwao. Tchambule anasema hadhira yao ilianza kufuatilia kwa haraka.
Gazeti la Evidencias
Reginaldo Tchambule, Mhariri wa Evidencias anasema: “Gazeti la Evidencias linaweza kuwa limepata muonekano na umaarufu mkubwa katika muda mfupi, kwa sababu ya jinsi tulivyozingatia uandishi wa habari wenyewe. Wakati fulani tulikuwa na ukurasa ambapo tulichunguza habari kuu zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.”
Mwaka huu, Tchambule aliripoti kwa nini Ossufo Momade, kiongozi wa Renamo, chama kikuu cha upinzani cha Msumbiji, hajaonekana hadharani kwa wiki kadhaa wakati wa kampeni za urais.
Uchunguzi wa Picha Mtandao wa Facebook
Evidencias ilianza kuchunguza picha kwenye mtandao wa Facebook wa mgombea ambapo ilionekana Momade alikuwa akifanya kazi nje ya nchi.
Tchambule anafafanua: “Tayari tulikuwa na mawasiliano na baadhi ya vyombo vya uthibitisho wa picha, tukaichukua na kuiweka kwenye programu na kugundua kuwa, picha hiyo ilikuwa imechapishwa kwenye ukurasa huo huo 2019, hiyo ikabadilisha mtazamo ambao ungeweza kuupotosha kwa umma.”
Pamoja na kuenea kwa taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii, Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA), mwandishi wa habari wa Msumbiji Armando Nhantumbo anasema uwekezaji katika teknolojia unahitajika kwenye vyumba vya habari kuelekeza wanahabari jinsi ya kukabiliana na upotoshaji pamoja na habari za uongo.
Taasisi ya MISA
Armando Nhantumbo wa Media Institute of Southern Africa anaeleza:
“Shukrani kwa teknolojia, tunapata taarifa zaidi, na tunaweza kushiriki zaidi na zaidi katika masuala ya utawala ambayo ilikuwa ngumu miaka 30 iliyopita. Kinachotokea ni pamoja na faida hizi, lakini kuna hasara pia. Mojawapo ya ubaya ni kutoijua habari.”
MISA Msumbiji
MISA Msumbiji inatoa huduma za kuangalia ukweli na kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari, Nhantumbo anasema.
Nhantumbo wa Media Institute of Southern Africa anasema:
“Kuna vyombo vya kidijitali vinavyotusaidia kufanya hili na sisi MISA Msumbiji tumekuwa tukiandaa mafunzo kwa wanafunzi wa uandishi wa habari, waandishi wa habari na mashirika ya kiraia juu ya jinsi ya kutumia majukwaa haya.”
Kwa vile jamii inategemea zaidi mitandao ya kijamii kwa habari, watetezi wa vyombo vya habari wanasema kazi kama ya Evidencias na MISA Msumbiji itakuwa chombo chenye nguvu katika kuhabarisha umma kwa usahihi na uwazi.
Ripoti ya Amarilis Gule VOA Maputo.