Somalia: Waandishi habari wahofia ukandamizaji wakati huu wa janga la Corona

Waandishi wa habari nchini Somalia.

Waandishi wa habari nchini Somalia wamesema kwamba kwa kawaida, huwa wanakabiliana na changamoto nyingi lakini  sasa, wakati huu wa janga la Corona, wanahofia ukandamizaji hata zaidi, ikiwa ni pamoja na kukamatwa kwa amri za baadhi ya viongozi wa kisiasa.

Wakati wakiadhimisha kimya kimya siku ya uhuru wa uanahabari ulimwenguni Jumapili, baadhi yao walizungumza na VOA wakieleza masaibu wanayopitia.

Mohamed Ibrahim Moalimu ambaye ni katibu wa taasisi ya waandishi habari wa Somalia alisema kuwa wanahabari watatu wamezuiliwa kwenye sehemu tofauti za taifa wakituhumiwa kufanya uhalifu huku kituo kimoja cha radio kinachotangaza kwa lugha ya Kisomali kikifungiwa kupeperusha matangaza tangu katikati ya mwezi uliopita.

Moalimu alisema kuwa ukandamizaji dhidi ya waandishi wa habari hasa wakati huu wa janga la corona ni lazima ukomeshwe.

Wanahabari nchini humo wanasema kuwa wanahatarisha maisha yao wakati wa kuripoti masuala yenye utata yanayohusu umma.

Serikali ya Somalia imekuwa ikikanusha madai ya kukandamiza wanahabari mara nyingi ikidai kuwa wanaripoti habari zisizo sahihi.

-Imeandikwa na Harrison Kamau, VOA, Washington DC