Waandamanaji wavamia bunge la Namibia

Bendera ya Namibia

Karibu waandamanaji 300 wamevamia bunge la Namibia Jumanne, wakati lilipokuwa likijianda kupitisha msaada wa dola billioni 1 wa Ujerumani kama fidia kutokana na mauaji ya kimbari dhidi ya Wanamibia wa kabila la Herero na Nama yaliyotekelezwa na Ujerumani kati ya mwaka wa 1904 na 1908.

Tarehe 28 mwezi Mei, viongozi wa Namibia walitangaza kwamba Ujerumani imekubali kufadhili miradi katika taifa hilo la kusini magharibi mwa Afrika, yenye thamani ya kiwango hicho cha dola billioni 1 katika kipindi cha miaka 30, kufuatia mauaji ya kuangamiza na kupokonya mali katika nchi hiyo ambayo ilikuwa chini ya ukoloni wa Ujerumani, zaidi ya karne moja iliyopita.

Ujerumani iliomba msamaha Mei 28 kwa kuhusika kwake katika mauaji ya watu wa kabila la Herero na Nama na kuyaelezea rasmi kwa mara ya kwanza kama mauaji ya kimbari.

Waandamanaji wakiongozwa na upinzani na viongozi wa kijadi kutoka jamii zilizoathiriwa, waliandamana kupitia mji mkuu Windhoek kabla ya kupanda juu ya uzio ili kuingia ndani ya jengo la bunge, wakisema kiwango cha fidia ni kidogo sana na wakipinga kwamba hawakushirikishwa katika mazungumzo na Ujerumani.