Waandamanaji Sudan wanaendelea kudai utawala wa kiraia

Waandamanaji Sudan katika mfungo wa Ramadan

Umati ulikusanyika nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum kwa Iftar ya kwanza ya Ramadan huku watu wakieleza dhamira ya kuendelea na maandamano bila kujali hali ya hewa ya joto kali au saumu kuwavunja nguvu

Waandamanaji wa Sudan siku ya Jumatatu walianza siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadan kwa kuapa kuendelea kushinikiza kampeni yao kwa ajili ya utawala wa kiraia.

Umati ulikusanyika nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum kwa Iftar ya kwanza ya Ramadan huku watu wengi wakieleza wanadhamira ya kuendelea na maandamano bila kujali hali ya hewa ya joto kali au saumu kuwavunja nguvu.

Wakati huo huo shirika la habari la serikali lilieleza Jumatatu kwamba polisi waligundua na kuchukua mikanda ya milipuko ikiwemo bunduki zikiwa na chombo cha sailensa, vifaa vinavyotumika kutegua milipuko kwa mbali na simu za satelaiti walipovamia nyumba moja katika mji mkuu Khartoum. Haikufahamika kama shehena hiyo ya silaha zilizopatikana zilikuwa na uhusiano kwa njia yeyote na matatizo ya kisiasa ya hivi sasa nchini humo.

Shirika hilo la habari halikueleza kama kuna mtu yeyote aliyekamatwa au mtu aliyemiliki silaha hizo. Rais aliyetawala kwa miaka 30 nchini humo Omar al Bashir aliondolewa madarakani na jeshi mwezi uliopita kufuatia miezi kadhaa ya maandamano ya kuupinga utawala wake.