Baadhi ya waandamanaji wa Sudan waliendelea Jumapili kukaa nje ya wizara ya ulinzi huku wakishinikiza jeshi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia. Mkuu wa baraza la jeshi ambaye alichukua nafasi ya rais wa zamani wa nchi hiyo Omar al Bashir aliyeondolewa madarakani Alhamis iliyopita baada ya kutawala kwa miaka 30 anasema serikali ya kiraia itaundwa baada ya mashauriano na upinzani.
Sauti ya Amerika-VOA ilizungumza na mkazi wa Sudan na kutaka kujua hali ya usalama mitaani ikoje wakati mashauriano ya kisiasa bado yanaendelea kati ya jeshi na viongozi wa upinzani.
Your browser doesn’t support HTML5
Waandaaji wakuu wa maandamano yaliyopelekea kuondolewa Bashir, umoja wa wasomi Sudan-SPA unadai kwamba raia wanatakiwa kushirikishwa kwenye baraza la mpito la kijeshi na wanashinikiza washirika wa karibu na Bashir kuondoka kwenye baraza hilo.
SPA wanataka serikali ya mpito ya kiraia itakayotawala kwa miaka minne ili kutayarisha demokrasia kamili nchini humo. SPA pia Inatoa wito wa kuundwa tena kwa mfumo wa madaraka kwenye idara ya taifa ya usalama na ujasusi-NISS na kuvunjwa kwa vikosi vya jeshi ambavyo vilifanya kazi chini ya Bashir.