Kashfa ya NYS: Waandamanaji Kenya washinikiza 'tunataka fedha zetu'

Wananchi wa Kenya wameandamana mjini Nairobi Alhamisi baada ya kudhihirika kuwa zaidi ya dola milioni 100 ya fedha za umma zilikuwa zimeibiwa.

Maandamano hayo yamekuja siku moja baada ya wafanyakazi wa serikali na wafanyabiashara 24 walipofunguliwa mashtaka ya wizi mahakamani kutokana na ufisadi huo.

Wakiwa wamevalia fulana nyekundu, wakiimba “tunataka pesa zetu zirejeshwe,” waandamanaji hao waliingia mitaani katika mji mkuu, Nairobi, kufikisha ujumbe wa hasira zao kutokana na ufisadi ulioikumba taasisi ya Huduma ya Vijana ya Taifa (NYS) nchini humo.

Hii ni kashfa ya pili katika kipindi cha miaka mitatu kuikumba taasisi hiyo, ambayo hutoa mafunzo yakuwawezesha vijana kupata kazi na kutoa huduma nyingine .

Katika matukio yote mawili, wafanyakazi wanahusika na manunuzi ya mahitaji ya miradi ya NYS inadaiwa kuwa walihamisha mamilioni ya dola kwenye akaunti zao binafsi katika mabenki.