Vyama vyatangaza kushiriki uchaguzi wa marudio Zanzibar

Vyama 12 visivyokuwa na wabunge Alhamisi vimetangaza kushiriki Uchaguzi wa marudio siku ya Jumapili, Machi 20, mwaka huu visiwani Zanzibar.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, baadhi ya viongozi wa vyama hivyo wamesema wameamua kushiriki kwa vile uchaguzi ndio njia pekee ya kuwapata viongozi kwa njia ya kidemokrasia

Vyama hivyo ni ADC, DP, CCK, SAU, AFP, TLP, ADA TADEA, UPDP, DEMOKRASIA MAKINI, NRA, UMD, na CHAUSTA.

Wakati huohuo, chama cha wananchi CUF kimelalamikia kilichodai matumizi ya nguvu pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na vyombo vya dola dhidi ya wanachama na wafuasi wake visiwani zanzibar wakati huu kuelekea uchaguzi wa marudio walioususia wa Jumapili.

CUF imedai polisi visiwani Zanzibar wamekuwa wakivamia wafuasi wa CUF majumbani na katika ofisi zao na kuwakamata kwa visingizo vya kuhusika na baadhi ya matukio ikiwemo milipuko iliyotokea Unguja na Pemba.

Naibu katibu mkuu wa CUF Tanzanaia Bara, Magdalena Sakaya, amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Alhamisi kuwa pamoja na chama cha CUF kutangaza kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio, inaonekana wafuasi wao wanatishwa ili kulazimishwa kwenda kupiga kura.

Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi wa Tanzania, Charles Kitwanga Jumatano alikuwepo visiwani Zanzibar ambapo katika mkutano wake na waandishi wa habari alisisitiza kuwepo kwa hali ya usalama visiwani humo kuelekea uchaguzi wa marudio Jumapili hii.

Tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilifuta uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana kwa madai ya kuwepo kasoro nyingi jambo lililozua mgogoro uliosababisha chama kikuu cha upinzani CUF kususia kushiriki marudio yaliyotangazwa kufanyika Jumapili hii Machi 20.