Vyama vya kislamu vyashinda uchaguzi Misri

Msemaji wa kundi la Muslim Brotherhood Mohammed Morsi akisalimiana na mwanajeshi baada ya kupiga kura yake mjini Cairo

Katika taarifa iliyotolewa na chama cha kislamu cha Freedom and Justice inaeleza kwamba kimeshinda viti 36 kati ya 56 vilivyotengewa wagombea huru.

Kundi kuu la kislamu la Misri lilidai Jumatano kwamba wanachama wake walinyakua viti vingi vya wagombea huru katika duru ya pili ya uchaguzi ulofanyika katika majimbo tisa pamoja na miji ya Cairo na Alexandria.

Chama cha Muslim Broitherhood kimeshapata ushindi mkubwa wa viti vilivyotengewa vyama vya kisaisa katika uchaguzi wa wiki iliyopita kikipata asili mia 37 za kura katika majimbo tisa kikifuatiwa na chama cha kihafidhina cha siasa kali cha Salafist kilichojipatia asili mia 24 za kura. Muungano wa vyama vya kiliberali umechukua nafasi ya tatu ukipata idadi ndogo zaidi ya kura.

Matokeo rasmi ya uchaguzi yanatazamiewa kutangazwa siku ya Alhamisi. Na ikithibitishwa kwamba Muslim Brotherhood kimeshinda viti vingi katika uchaguzi wa wagombea huru, basi kitakua chama chenye nguvu katika bunge la viti 498.

Wakati huo huo waziri mkuu wa mpito wa Misri Kamal el-Ganzouri alitangaza baraza jipya la mawaziri Jumatano akiwarudisha karibu mawaziri 12 wa serikali iliyopita.