Viongozi wa Umoja wa Ulaya Ijumaa wamekubaliana kumteua Ursula von der Leyen wa Ujerumani kwa muhula wa pili wa miaka mitano kama rais wa Tume ya Ulaya, chombo chenye nguvu cha utendaji cha EU.
Katika mkutano wa mjini Brussels, viongozi 27 wa umoja huo pia wamemchagua waziri mkuu wa zamani wa Ureno, Antonio Costa, kuwa mwenyekiti wa baadaye wa mikutano ya Baraza la Ulaya na kumchagua Waziri Mkuu wa Estonia, Kaja Kallas kuwa mkuu ajaye wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya.
Jopo la uongozi linawakilisha mwendelezo wa jumuiya hiyo yenye wanachama 27, huku mirengo inayounga mkono Umoja wa Ulaya ikishikilia nyadhifa za juu licha ya kuongezeka kwa mrengo wa kulia katika uchaguzi wa Bunge la Ulaya mapema mwezi huu.
Watatu hao waliungwa mkono na viongozi, lakini inadaiwa Waziri Mkuu wa Italia, wa mrengo wa kulia Giorgia Meloni hakumpigia kura von der Leyen ila alimpigia kura Costa na Kallas.