Visa vya surua vyaongezeka maradufu barani Ulaya

  • VOA News
Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa yanasema visa vya ugonjwa wa surua barani Ulaya vimeongezeka maradufu ikilinganishwa na mwaka uliopita, vikiongezeka hadi 127,000, idadi ya juu sana tangu mwaka 1997.

Ni sawa na theluthi moja ya visa vyote duniani.

Katika taarifa ya pamoja, ofisi za UNICEF na WHO kanda ya Ulaya na Asia ya Kati zimesema watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ni sawa na asilimia 40 ya wagonjwa katika kanda ya WHO barani Ulaya, ambayo inasimamia nchi 53.

Taarifa hiyo imesema zaidi ya nusu ya visa hivyo vilihitaji kulazwa hospitali. Ilisema pia kufikia tarehe 6 Machi mwaka huu, vifo 38 kutokana na surua vimeripotiwa.

Mashirika hayo yanasema visa vya surua katika kanda ya Ulaya vimekuwa vikipungua kwa kasi katika miongo miwili tangu 1997, vikishuka hadi 4,440 mwaka 2016, lakini viliongezeka tena kwa kiasi kikubwa tangu mwaka 2018.