Shirika la afya duniani-WHO linaonya kwamba virusi vya ZIKA vinavyoonekana kuwa na uwezo wa kusababisha madhara makubwa kwa mtoto vinasambaa haraka kote katika mabara ya Amerika na vitaweza kuathiri watu wapatao milioni nne.
WHO ilisema virusi hivyo vinavyotokana na mbu, awali vilionekana kama hatari isiyo kubwa kwa binadamu lakini virusi vimekuwa vikikua haraka na kuwa kitisho cha afya ya umma.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, Margareth Chan alisema virusi vya ZIKA viligunduliwa nchini Uganda mwaka 1947 lakini tangu wakati huo vimesambaa kote duniani na katika miaka ya karibuni vimekuwa vikihusishwa na matatizo ya fahamu mwilini.
Maelfu ya wanawake wajawazito walioathiriwa na virusi hivi vya ZIKA wameanza kupata matatizo wakati wa kujifungua au kujifungua watoto walemavu.