Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer Alhamisi alifungua mkutano wa Jumuia ya kisiasa ya Ulaya katika Jumba la Blenheim karibu na Oxford na wito kwa Ulaya kuthibitisha uungaji mkono wake kwa Ukraine na kuungana dhidi ya uvamizi wa Russia.
“Kwa sababu tishio la Russia limefika barani Ulaya kote,” Starmer alisema, “Wengi kati yetu mlishuhudia mashambulizi dhidi ya demokrasia yetu. Watu wakilengwa mitaani kwetu.
Ndege za kijeshi zikiingia kwenye anga yetu. Meli zikifanya doria katika maeneo yetu ya pwani,” alisema, akiongeza “ huu ni wakati kwetu sote kufanya mengi zaidi.”
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, mgeni mkuu katika mkutano huo, alizungumza mara tu baadaye, na kupongeza uungwaji mkono wa Ulaya kwa nchi yake, akisema, “Putin hawezi kuendeleza uhusiano na viongozi wakweli wenye nguvu. Na hii ndio faida yetu.”
Lakini Zelenskiy alionya “Itaendelea kuwa faida iwapo tu tutakuwa tumeungana.”