Viongozi wa SADC na EAC wakutana Tanzania kujadili mzozo wa DRC

Rais wa Rwanda, Paul Kagame, na mwenzake wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tshisekedi, walishiriki mkutano wa Jumamosi, Tanzania, ambapo viongozi wa kikanda walitoa mwito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano nchini DRC.

Kundi la waasi wa M23, linaloungwa mkono na Rwanda limeteka maeneo mengi katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini mashariki mwa DRC katika mashambulizi ambayo yamesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na idadi kubwa ya watu kuyahama makazi yao.

Kundi hilo lilichukua mji wa kimkakati wa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, wiki iliyopita, lilidai kuelekea jimbo jirani la Kivu Kusini.

Jumamosi, mapigano yaliendelea takriban kilomita 60 kutoka mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, Bakuvu, vyanzo vya ndani na usalama vimeiambia AFP.