Meya wa Kyiv Vitali Klitschko aliandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba kulitokea mlipuko katika wilaya ya kati ya Podil.
Baadaye Klitschko alisema kwamba milipuko iliyosikika mjini Kyiv ilisababishwa na mifumo ya ulinzi wa anga karibu na mji mkuu.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ni miongoni mwa ujumbe huo wa Umoja wa Afrika ambao unakutana na Rais wa Ukraine Volodymr Zelenskiy, hatua ya kwanza katika jukumu la kutafuta makubaliano ya amani kati ya Kyiv na Moscow.
Wajumbe wengine ni Rais wa Senegal Macky Sall, Rais wa Zambia Hakainde Hichilema na Rais wa Comoros Azali Assoumani, ambaye ndiye mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika.
Marais wengine watatu, wa Jamhuri ya Congo, Misri na Uganda walitarajiwa kushiriki katika ujumbe huo lakini badale yake walituma wawakilishi.
Baada ya kukutana na Rais Zelenskiy leo Ijumaa, marais hao watasafiri kuelekea Russia kukutana na Rais Vladimir Putin.