Utawala mpya wa kijeshi, ambao ulimuondoa rais wa Niger aliyechaguliwa kidemokrasia miezi miwili iliyopita, ulisema katika taarifa iliyotolewa usiku wa kuamkia leo kwamba ratiba ya kuondoka kwa wanajeshi hao lazima ijumuishwe kwenye mkakati na kwa makubaliano ya pande zote.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron siku ya Jumapili alitangaza kwamba Ufaransa itamuondoa balozi wake nchini Niger, na kuondoa baadaye kikosi cha wanajeshi wake katika miezi ijayo.
Alisema ushirikiano wa kijeshi “umemalizika” na kwamba wanajeshi wa Ufaransa wataondoka katika “miezi na wiki zijazo”, na kukamilisha mchakato huo mwishoni mwa mwaka huu”.
Ufaransa ina wanajeshi 1,500 katika koloni lake la zamani kama sehemu ya kikosi cha kupambana na wanajihadi katika eneo la Sahel.