Viongozi wa Jumuiya ya Uchumi wa Afrika Magharibi (ECOWAS) wameamuru kuanzishwa kwa mpango wa kupeleka jeshi katika kuhakikisha kuurejesha utawala wa kidemokrasia na Rais Bazoum aliyepinduliwa na jeshi Julai 26.
Uamuzi huo umeelezewa katika maazimio yaliyofikiwa Alhamisi baada ya majadiliano ya viongozi wa ECOWAS juu ya hali ya kisiasa nchini Niger katika mkutano wao wa pili. Viongozi hao walikutana mjini Abuja, Nigeria.
Mwanzoni mwa mkutano huo viongozi hao walielezea umuhimu wa kutatua suala la mapinduzi nchini Niger, viongozi hao walitoa onyo kali na kukemea mapinduzi au mabadiliko ya serikali kinyume na katiba, waliazimia kuhakikisha kuwa mapinduzi hayaruhusiwi tena Afrika Magharibi.
Akiwasilisha taarifa ya mkutano huo Rais wa tume ya ECOWAS Omar Toure aliwaambia waandishi wa habari kwamba viongozi hao hawakufurahishwa na majibu ya utawala wa kijeshi huko Niger kukataa kukutana na wajumbe wa ECOWAS waliotumwa kuzungumza nao kuhusu hatua za kuchukuliwa ili suluhu ipatikane kwa ajili ya nchi hiyo.
Omar Toure anasema viongozi hao wameamuru kutekelezwa kwa maazimio ya mkutano uliofanyika Abuja Julai 30 pamoja na uamuzi wa matumizi ya nguvu kurejesha demokrasia katika Jamhuri ya Niger.
Toure anasema viongozi wa ECOWAS wameamuru Kikosi cha Usalama cha ECOWAS kupeleka wanajeshi nchini Niger kurejesha utaratibu wa kikatiba huko jamhuri ya Niger.
Hivi sasa inaelezewa kuwa Rais Bazoum amekubali kujiuzulu na kupisha nguvu ya jeshi.
Hali ya kisiasa nchini Niger imeongeza hofu kuhusu ukosefu wa usalama katika eneo la kaskazini mwa Nigeria na watu wanaoishi maeneo ya mpakani wameanza kuhama kuelekea kusini mwa nchi kwa ajili ya uwezekano wa kushambuliwa na magaidi.
Wachambuzi wanasema uwezekano wa kuingilia kati kijeshi unaweza kuiumiza pia Nigeria kwa namna fulani.
Waziri zamani wa mambo ya nje wa Nigeria pia mtaalamu wa uhusiano wa kimataifa, Profesa Nurudeen Mohammed anasema siku hizi ECOWAS haina nguvu au uwezo kama zamani kwa hivyo viongozi wa kijeshi wa jamhuri ya Niger waliweza kukataa kuwaona wajumbe waliotumwa na ECOWAS kuzungumza nao.
Mkutano wa Alhamisi mjini Abuja ni wa pili kwa viongozi wa Afrika Magharibi katika jitihada zao za kutatua tatizo la kisiasa ambalo limesababishwa na kupinduliwa kwa serikali ya kiraia huko jamhuri ya Niger.
Na uamuzi wa kupeleka vikosi vya jeshi la ECOWAS huko Niamey kurejesha demokrasia na utawala wa kikatiba kunaweza kuwa na mapambano ya muda mrefu ya kuchukua madaraka ambayo hakuna anayejua yataisha lini.