Viongozi wa dunia wanaelezea uungaji mkono wao kwa watu wa Cuba baada ya maandamano ya Jumapili kote kwenye kisiwa hicho.
Waziri wa mambo ya nje wa umoja wa ulaya, Josep Borrell, aliisihi serikali ya Cuba “kusikiliza maandamano haya yanayodai kutoridhika” akiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari hapo Jumatatu huko Brussels baada ya kukutana na mawaziri wa mambo ya nje wa EU.
Erica Guevara-Rosas, mkurugenzi wa Marekani kwenye Amnesty International, aliyaita maandamano ya Jumapili, siku ya kihistoria kwa Cuba, wakati akielezea wasi wasi wake juu ya ripoti za kuzimwa kwa mtandao, ukamataji holela, matumizi ya nguvu kupita kiasi, ikijumuisha polisi kuwafyatulia risasi waandamanaji, pamoja na orodha ndefu ya watu kupotea.
Guevara-Rosas alitoa wito kwa Rais wa Cuba, Miguel Diaz-Canal na serikali yake kushughulikia madai ya kijamii ya raia wake kutokana na matatizo ya kiuchumi, uhaba wa chakula na dawa, kuporomoka kwa mfumo wa afya, ambao haujibu hali ya sasa ya tatizo la COVID-19, na lundo la madai ya kihistoria kwa kuheshimu haki za uhuru wa kujieleza na mikusanyiko wa amani.