Viongozi wa Chadema wahukumiwa kifungo Tanzania

Rais John Magufuli

Mara baada ya Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu kuhukumiwa Jumatatu yeye na Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Emmanuel Masonga kwenda jela kila mmoja ezi mitano wakili wao amekata rufaa.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya imewakuta na hatia ya kumkashifu Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli.

Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimeripoti kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite ametoa hukumu hiyo leo saa tatu asubuhi.

Wakati kesi hiyo inaamuliwa wakili wa washitakiwa, Peter Kibatala aliiomba mahakama kutoa adhabu mbadala lakini upande wa mashtaka uliiomba Mahakama itoe adhabu kali ili liwe fundisho kwa watu wengine, kwa madai ya kuwa kauli zao zimemfedhehesha rais. Lakini mahakama ilikubaliana na maelezo ya upande wa mshtaka.

Sugu na Masonga walikuwa wanakabiliwa na shitaka moja la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli katika mkutano wa hadhara wa Mbunge huyo, uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge mwezi Disemba 2017.

Januari 16, mwaka huu washitakiwa hao, walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa shitaka moja la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hati ya mashtaka imeeleza kuwa kauli waliotumia ilikuwa inakiuka kifungu cha 89(1) cha Sheria za Jinai ambayo inaharamisha kutumiwa kwa lugha ya matusi.

Maneno hayo, hati za mashtaka zinaeleza kuwa yangeweza kusababisha uvunjifu wa amani.