Afrika Mashariki yadhamini kuisuluhisha Sudan Kusini

Watoto waliokimbia vita Sudan Kusini wakiwa katika eneo la Kambi ya wakimbizi ya Bidi Bidi kaskazini ya Uganda.

Viongozi wa Afrika Mashariki wamesema jumatatu kuwa watajaribu kuzileta pamoja pande zinazozozana Sudan kusini kwenye meza ya mazungumzo kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa nchi hiyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya mazungumzo hayo kuvunjika pamoja na kuahirishwa uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika Agosti mwaka ujao na kutafuta tarehe mbadala.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, viongozi hao wanaokutana Addis Ababa Ethiopia wanapanga kuunda kikao kitakacho waleta mahasimu pamoja.

Hizo ni juhudi za kusitisha mapigano yaliochochewa na ukabila kwa zaidi ya miaka 3 na kusababisha uhaba mkubwa wa chakula.

Mapigano yalizuka sudan kusini 2013 baada ya rais Salva Kiir kumfukuza kazi naibu wake Rieck Machar miaka miwili tu baada ya taifa hilo kupata uhuru kutoka kwa Sudan.

Baada ya hatua kadhaa za mazungumzo ya Amani kufeli, Kiir na Machar walitia saini makataba wa kugawana madaraka agosti 2015 na kukubaliana kuunda serikali ya mpito na hatimae kuitisha uchaguzi. Lakini makataba huo ulivunjika na kupelekea Machar kutoroka nchini.