“Kile kilichotokea leo mjini Washington, DC, siyo utamaduni wa Marekani,” Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema katika ujumbe wa video kupitia akaunti yake ya Twitter Jumatano. “Tunaamini katika nguvu ya demokrasia yetu. Tunaamini katika nguvu ya demokrasia ya Marekani.”
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alisema “amesikitishwa” kuona “ghasia na fujo” zilizo tokea Washington katika taarifa yake kwenye Twitter. “Kukabidhiana madaraka kwa amani na utulivu lazima kuendelee. Mchakato huu wa kidemokrasia hauwezi kuruhusiwa kukandamizwa na maandamano yanayo kiuka sheria.”
Wizara ya Mambo ya Nje wa Taiwan imeelezea masikitiko yake juu ya ghasia katika tamko ililolitoa Alhamisi. Wizara hiyo imesema imetuma ujumbe wa dharura kwa raia wa Taiwan “kuwa waangalifu zaidi na kuhakikisha usalama wao” kufuatia amri ya kutotoka nje usiku iliyotangazwa na maafisa wa jiji la Washington.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistani Zahid Hafeez Choudhri amewaambia waandishi wa habari Alhamisi kuwa serikali inafuatilia kwa karibu matukio ya Washington. “Nimatumaini yetu kuwa hali itakuwa shwari mara moja na haitaathiri mchakato wa kukabidhiana madaraka,” amesema Choudhri.
Shariman Lockman, mchambuzi mwandamizi wa sera za mambo ya nje na masuala ya usalama katika Taasisi ya Mikakati na Utafiti wa Kimataifa Malaysia, ameiambia VOA ghasia hizi “ haziiweki Marekani katika picha nzuri duniani.”
“Inaongeza fikra hasi ambazo watu tayari wanazo juu ya Marekani. Unajua, huwezi kudhibiti COVID na pia huwezi kuendesha uchaguzi sawasawa. Nyie [serikali ya Marekani] mnaendelea kutuambia vipi tujipange, lakini nyie hamuwezi kujipanga sawasawa.”
Huko Korea Kusini, mbunge mwandamizi Song Young-gil, wa Chama tawala cha Democratic, alisema katika ujumbe wake wa Facebook ghasia hizo “ zimedhihirisha fedheha kwa upande wa Marekani.”
“Tabia ya aina hii inaweza kutumiwa na viongozi wa kiimla ambao wanataka kuhalalisha mwenendo wao,” ameongeza Song, ambaye hakufafanua. “Natarajia kuona Marekani ikiimarisha mfumo wake.”
“Matukio ya kusikitisha katika Bunge la Marekani. Marekani inasimamia demokrasia ulimwenguni na hivi sasa ni muhimu kuwepo kukabidhiana madaraka kwa amani na utulivu,” Waziri wa Mkuu wa Uingereza Boris Johnson aliandika katika ujumbe wake wa Twitter.
Maafisa wa Umoja wa Ulaya walieleza kumuunga mkono Biden Jumatano, wakati wale wenye msimamo mkali wanaomuunga mkono Trump walilazimisha kufungwa kwa jengo la Bunge la Marekani, wakivuruga utaratibu wa kumrasmisha Joe Biden kuwa mshindi wa urais.
“Ninaamini nguvu za taasisi za Marekani na demokrasia yake. Kukabidhiana madaraka kwa amani ni suala la msingi. @JoeBiden ameshinda uchaguzi,” Ursula von der Leyen, rais wa Tume ya Ulaya, aliandika kupitia Twitter.
“Matokeo ya uchaguzi huu wa kidemokrasia lazima yaheshimiwe,” Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg ameandika katika ujumbe wa Twitter.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imetoa taarifa Jumatano ikiwasihi raia wake nchini Marekani kuepuka sehemu mikusanyiko na malumbano.
“Tunataka pande zote Marekani kutumia uvumilivu na busara. Tunaamini kuwa Marekani itapata ufumbuzi wa mgogoro huu wa kisiasa ndani ya nchi kwa kutumia uzoefu,” imeandika katika tamko lake.
Jumuiya ya nchi za mataifa ya Amerika pia zimelaani ghasia hizo.
Vitendo vya kutumia nguvu na uharibifu dhidi ya taasisi zinapelekea upigaji vita dhidi ya harakati za kidemokrasia,” Sekretariet ya nchi za OAS inayoangazia matukio imeandika katika tamko lake Jumatano, ikisisitiza umuhimu wa kutumika busara.
Katika hotuba yake kupitia televisheni Alhamisi, Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema uvamizi uliotokea katika Bunge la Marekani ni ushahidi wa udhaifu wa demokrasia ya nchi za Magharibi na unaweza kutekwa nyara na umashuhuri.
Amesema, “Mtu mashuhuri amewasili, na kuiongoza nchi yake katika balaa kwakipindi cha miaka minne hii.”
Rohani ameongeza ana matumaini “ wanaokuja kuingia White House” watarejesha hadhi ya nchi hii katika nafasi yake muhimu kama taifa la Marekani, kwa sababu taifa la Marekani ni taifa muhimu.”